Bunge la Katiba-Mjadala wa Rasimu-Siku ya tatu


Leo mjadala wa rasimu umeendelea. Kwa mujibu wa kanuni, kamati zilitakiwa kujadili sura mbili kwa siku mbili. Pamoja na kuongeza siku, baadhi ya kamati zimemaliza kazi na nyingine zimeshindwa kukamilisha kazi hii ndani ya muda uliopangwa.

Tulitarajia kuwa kesho uwasilishaji wa taarifa za kamati ungefanyika Bungeni, lakini kuna dalili zote kuwa Bunge kesho litahairishwa ili kupisha kamati kumaliza kazi zao.

Sura ya kwanza na ya sita zimebeba muundo wa Serikali. Sura hizi ndizo zenye mvutano mkali. Tukifanikiwa kukubaliana kwenye sura hizi, tunatarajia sura nyingine zinaweza kwenda kwa kasi zaidi.

Uwezekano wa kumaliza kazi ya kujadili rasimu ya katiba hii ni mdogo. Kuna uwezekano mkubwa kwa Bunge la Katiba kuahirishwa ili kupisha Bunge la Bajeti kukaa na kupitia Bajeti ya Serikali. Vile vile kuna uwezekano tukashindwa kuendelea iwapo pande zote za Muungano zitashindwa kupata 2/3 ya kura zinazohitajika kupitisha ibara mbali za Katiba.
Wiki mbili au tatu zijazo zitatoa picha halisi ya mchakato huu.

Tuendelee kuwa pamoja.

Posted in Uncategorized | Tagged , , , , | Leave a comment

Bunge la Katiba- Mjadala wa Rasimu-Siku ya Pili


Leo mjadala wa rasimu ya katiba umeendelea, huku mvutano ukiwa katika muundo wa Muungano na vile vile kwa baadhi ya wajumbe kutaka kupatiwa nakala za hati ya Muungano na ushahidi wa kuridhiwa kwa Muungano upande wa Zanzibar. Hata hivyo, vielelezo hivi havikutolewa.

Mzee Pius Msekwa ambaye alikuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati Muungano naye alipata fursa ya kutembelea baadhi ya kamati na kutoa ushuhuda wa matukio mbali mbali kabla na baada ya Muungano.

Tulitarajia kumaliza kupitia sura ya kwanza na sita kesho, lakini kutokana na kazi kuwa kubwa, kesho tutaendelea na kazi hiyo. Kamati nyingi zipo katika ngazi ya kupiga kura, huku mwelekeo unaonyesha Muungano wa Serikali mbili kupewa nafasi zaidi na kuungwa mkono na wengi.

Kesho tunatarajia kukamilisha kazi ya kujadili sura ya kwanza na sita.

Posted in Uncategorized | Tagged , , , , | Leave a comment

Bunge la Katiba-Mjadala wa Rasimu- Siku ya kwanza


Baada ya zaidi ya siku thelathini baada ya Bunge la Katiba kuitishwa rasmi Dodoma tarehe 18 Februari 2014, leo tumeanza kujadili rasimu ya katiba.
Ikumbukwe hapo awali tulikuwa tumelenga kuwa na katiba mpya ifikapo tarehe 26 Aprili, 2014 siku ambayo tunaadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Zoezi la kuandaa kanuni limetuchukua muda mrefu sana kutokana na mvutano uliokuwepo katika makundi mbalimbali. Hata hivyo, suala la upigaji kura, tumeshindwa kufikia muafaka na hivyo kuamua kutumia kura za siri na wazi kwa wakati mmoja.

Leo uchambuzi wa rasimu ya katiba umeanza rasmi kwa kupitia sura ya kwanza na sita. Sura hizi ndio zinazobeba muundo wa Serikali. Inabidi tuamue hili kwanza kabla ya mambo mengine kujadiliwa. Kamati zote kumi na mbili zimejadili sura hizi mbili.

Siku ya leo imekuwa na mjadala mzito na mvutano kuhusu muundo na aina ya Muungano. Wapo waliokuwa wanashabikia Serikali mbili na waliokuwa wanapigia debe Serikali tatu. Kila msemaji alijaribu kujenga hoja kwa kutumia nyaraka mbalimbali ikiwa ni pamoja na randama ya Tume ya Katiba, rasimu ya katiba, majarida na vitabu mbalimbali.

Kilichojitokeza zaidi leo ni pamoja na ujengaji wa hoja bila kufanya utafiti wa kina; malumbano ya makundi ya kisiasa na ukosefu wa subira wa baadhi ya wajumbe kwa wachangiaji wenye mtazamo tofauti.

Kesho tutahitimisha mjadala wa sura ya kwanza na ya sita kwa kupiga kura.
Hitimisho la mjadala huu ndio utakuwa dira ya katiba inayopendekezwa.

Tukutane tena kesho kwa taarifa zaidi.

Posted in Uncategorized | Tagged , , , , | Leave a comment

Ziara yangu Ubalozini Bujumbura, Burundi


20131120-170621.jpg
Niko Jijini Bujumbura, nikiwakilisha Bunge la Tanzania katika Kongamano lililoandaliwa na Inter-Parliamentary Union (IPU) likiwa na lengo la kujengea uwezo Bunge la Burundi katika masuala ya UKIMWI.
Jana niliwasilisha mada kuhusu ushiriki wa Bunge la Tanzania katika masuala ya UKIMWI kupitia Kamati ya Bunge ya UKIMWI na Madawa ya Kulevya na Chama cha Wabunge dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI (TAPAC). Mimi ni mjumbe wa kamati hii na vile vile ni Katibu wa TAPAC.
Mchana wa leo, nilifika kwenye Ubalozi wetu hapa Bujumbura. Nilipokelewa vizuri na kuonana na Mheshimiwa Balozi Dr James Nzagi.
Tumeongea mambo mengi sana. Kuanzia hali ya kisiasa nchini Burundi, mchakato wao wa marekebisho ya katiba na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa nchi hii mwaka 2015. Nami nilimpa maelezo ya mchakato wa katiba na hali ya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Vile vile, nilimpongeza Mheshimiwa Balozi na Maofisa Ubalozi kwa uwakilishi mzuri wa nchi yetu.
Heshima ya Tanzania hapa Burundi ipo juu sana. Kila ninapokwenda ninapokelewa vizuri na kutumwa salamu kwa watanzania.
Jana nilikutana na Mbunge mmoja ambaye aliishi kama mkimbizi Kigoma kwa miaka kumi. Alisema anawashukuru watanzania kwa wema waliomtendea. Nilifarijika sana kuona Warundi wanatambua na kuthamini mchango wetu katika amani ya nchi hii.

Pichani: Kutoka kushoto : Bw Elias Tamba (Kansela), mdau na Mhe. Balozi Dr James Nzagi

Posted in Uncategorized | Tagged , , , , | Leave a comment

Ziarani Bujumbura, Burundi


20131120-165010.jpg
Benki ya CRDB imefungua tawi lake katika nchi ya Burundi. Tawi la Benki hii hapa Bujumbura lilianzishwa mwaka jana. Leo nilipata nafasi ya kutembelea Benki hii. Nimekutana na vijana wa kitanzania wanaopeperusha bendera ya Tanzania hapa Burundi. Nimeongea nao kuhusu matarajio ya benki hii, mafanikio na changamoto zinazowakabili. Nimefurahishwa na maelezo yao pamoja na huduma yao kwa wateja. Hakika kwa mwendo huu watapiga hatua. Pichani: makao makuu ya Benki hii.

20131120-165025.jpg
Juu: Picha ya pamoja na Uongozi wa Benki hii hapa Bujumbura, Burundi.

Posted in Uncategorized | Tagged , , | Leave a comment

Mfumo mpya wa madaraja ya ufaulu Tanzania.


20131031-214849.jpg
Serikali leo imetangaza mfumo mpya wa kupanga madaraja ya ufaulu kwa elimu ya Sekondari. Katika mfumo huu matumizi ya tathmini endelevu ya mwanafunzi (Continuous Assessment) itatumika katika kupata alama za mwisho (final grade).
Nini mtazamo wako kuhusu mfumo huu mpya? Je mfumo huu mpya unatatua changamoto za ufaulu? Elimu ni moja sekta iliyo kwenye Matokeo Makubwa Sasa( Big Results Now), vipaumbele viwe nini? Nakaribisha maoni!

Posted in Uncategorized | Tagged , , , , | Leave a comment

Barabara ya Kivukoni Front (Kivukoni-Utumishi) yafungwa


20131029-103021.jpg
Kipande cha barabara ya Kivukoni Front toka kwenye kivuko hadi Ofisi za Wizara ya Utumishi imefungwa ili kupisha ukarabati.
Hivi sasa magari yanayotoka kwenye kivuko yanatumia Barabara ya kuelekea soko la samaki Feri na kutokea Tume ya Mipango au barabara ya Barack Obama (zamani Ocean Road).
Kwa sasa kuna msongamano mkubwa kwenye barabara ya kuingia na kutokea kwenye kivuko. Haijulikani zoezi la kufunga barabara litaisha lini.
Natoa rai kwa wakazi wa Kigamboni kuepuka matumizi ya magari kama sio lazima katika kipindi hiki cha mpito.
Asanteni
Dkt Faustine Ndugulile
Mbunge Kigamboni

Posted in Uncategorized | Leave a comment