Buriani Mhe. Eugene Mwaiposa MB


Jana na leo si siku nzuri kwangu. Nikiwa njiani kuja Dodoma, nilipata ajali. Namshukuru Mungu niko salama lakini gari imeharibika sana baada ya kugongwa na Lori la aina ya Semi-trailer. Gari lilivutwa kurudi Dar nami niliendelea na safari ya Dodoma.

Nilipofika Dodoma, Mbunge wa kwanza kuonana naye alikuwa Mhe. Eugene Mwaiposa wa Ukonga. Tulikutana kwenye geti la kuingilia mjengoni. Tuliongea na kutaniana kuhusu michakato ya uchaguzi kwenye majimbo yetu.

Baada ya Bunge kuanza jioni alikuja akakaa kwenye kiti changu na kuongea na Mhe. Esther Bulaya. Aliniomba namba za simu za Waziri mmojawapo nikampa na alipohitimisha maongezi yake na Mhe. Bulaya alirudi kitini kwake. Hii ilikuwa kwenye saa kumi na moja jioni. Alionekana mzima na mwenye afya.

Leo asubuhi nikapata taarifa kuwa Mhe. Mwaiposa ametutoka. Nilishtuka sana.

Nitamkumbuka Mhe. Mwaiposa Kwa ushirikiano wake katika Umoja wa Wabunge wa Dar Es Salaam.

Umetangulia Mhe. Mwaiposa, nasi tuko njiani. Kapumzike kwa amani. 

Dkt Faustine Ndugulile MB

Mbunge wa Kigamboni

Posted in Uncategorized | 1 Comment

MREJESHO WA KIKAO CHA MASHAURIANO KUHUSU MPANGO KABAMBE WA UENDELEZAJI WA MJI MPYA WA KIGAMBONI KILICHO FANYIKA KATIKA UKUMBI WA CHUO CHA MWALIMU NYERERE, KIGAMBONI, TAREHE 10.08.2014


Posted in Uncategorized | Leave a comment

Sherehe ya kukabidhi madawati 650 kwa shule za sekondari za kata 12 Tarafa ya Mbagala


20140731-224528-81928359.jpg

20140731-224528-81928818.jpg

20140731-224529-81929269.jpg
1. Mbunge wa Kigamboni,Dk Faustine Ndugulile, akiangalia madawati kabla ya kukabidhi madawati 650 yenye thamani ya Tsh 69 millioni ,makabidhiano yaliyofanyika katika shule ya sekondari Mbagala.
2.MBUNGE wa Kigamboni,Dk Faustine Ndugulile, akikata utepe kuashiria tendo la kukabidhi madawati 650.
3.MBUNGE wa Kigamboni,Dk Faustine Ndugulile, (katikati),akiwa na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya manispaa ya Temeke idara ya elimu, mara baada ya kukabidhi madawati 650 kwa shule 12 za sekondari katika tarafa ya Mbagala jijini Dar Es Salaam.

Posted in Uncategorized | Tagged , , , , | Leave a comment

Ujenzi wa miundombinu Zakhem-Kingugi


20140629-120839-43719218.jpg

20140629-120838-43718607.jpg
Barabara isiyo rasmi ya Zakhem-Kingugi ni njia inayotumika na wakazi wengi wanaoishi maeneo ya Kingugi na Kilungule.
Kwa sasa wakazi wenye magari wanaokwenda Kingugi hutumia njia ya mzunguko kupitia Corner Bar.
Ujenzi wa Box Culvert umeanza na Manispaa imetenga zaidi ya Tsh 100million kwa ajili ya kutengeneza barabara hii.
Naushukuru sana uongozi wa Tazama Pipeline kwa ushirikiano walionipa mimi na Manispaa katika kuanisha eneo la kujenga Daraja na barabara. Ikumbukwe kuwa eneo hili ni sehemu ya hifadhi ya kupitisha bomba la mafuta. Lakini kutokana na mahusiano mazuri kati ya Tazama Pipeline na sisi, wamekubali tujenge Daraja hili na barabara ambayo itakuwa ni mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Kingugi na Kilungule.

Posted in Uncategorized | Tagged , , , , , | Leave a comment

Mrejesho wa suala la umeme kwa maeneo mbalimbali ya Jimbo la Kigamboni


Siku ya Jumatatu tarehe 23.06.2014 nilifanya mkutano na uongozi wa Tanesco ngazi ya Mkoa wa Temeke na Wilaya ya Kigamboni. Mambo yaliyojadiliwa ni pamoja na:

  1. Kukatika kwa mara kwa mara kwa umeme 
  2. Umeme mdogo kwa baadhi ya maeneo 
  3. Uunganishaji wa umeme kwa wateja wapya
  4. Miradi mipya ya umeme kwa Jimbo la Kigamboni

1. KUKATIKA KWA MARA KWA UMEME JIMBO LA KIGAMBONI

Umeme unaopatikana kwa wateja wa Jimbo la Kigamboni unatoka sub-station ya Ilala. Umeme huu pia husambazwa kwa maeneo ya Temeke, Mbagala na Mkuranga. Kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji pamoja na uchakavu wa miundombinu, kumekuwa na ukatikaji wa umeme mara kwa mara.

Tanesco walinieleza kuwa hatua ambazo wanachukua kuondoa tatizo hili ni pamoja na maboresho ya miundombinu, kusafisha njia unaopita umeme huo kwa kukata miti na matawi na kujenga sub-station mpya maeneo ya Mbagala. Kukamilika kwa sub-station ya Mbagala utapunguza utegemezi uliopo sasa kwa sub-station ya Ilala. Kazi ya ujenzi wa sub-station mpya unatarajia kukamilika mwezi Disemba mwaka huu.

2. UMEME MDOGO KWA BAADHI YA MAENEO (LOW VOLTAGE)

Kuna baadhi ya maeneo kama vile Kijichi na Magogoni kumekuwa na tatizo la umeme mdogo. Tanesco walinitaarifu kuwa kuna mpango wa kufanya “voltage improvement” kwa kufanya “phase addition” na kuongeza transfoma nyingine mbili maeneo ya Magogoni. Transfoma zipo na ninatarajia kazi hii itaanza hivi karibuni. Kwa upande wa Kijichi, pamoja na “voltage improvement” bado kutakuwa na tatizo. Suluhu ya kudumu itakuwa kukamilika kwa sub-station ya Mbagala.

Tulikubaliana kuwa kazi hii iwe imekamilika ndani ya miezi mitatu ijayo.

3. UMEME KWA WATEJA WAPYA

Nimekuwa nikipokea malalamiko mengi toka kwa wananchi wengi ambao wamekuwa wakisubiri muda mrefu kupata huduma ya umeme. Malalamiko yamekuwa yakitoka Kibada, Gezaulole, Toangoma, Saku, Rufu na Kiponza.

Uongozi wa Tanesco ulinihakikishia kuwa maandalizi yamekamilika kwa ajili ya usambazaji wa umeme kwenye maeneo ya Kibada (blocks 14,15,16,17,18,19,20).  Waliahidi kukamilisha kazi hii ifikapo mwezi Septemba 2014.

Niliwataka ndani ya wiki tatu (3) kunipa mikakati yao ya kuwapatia umeme wananchi walioomba toka maeneo ya Gezaulole, Mbwamaji, Kizani, Mwera, Kibada(blocks zilizobaki), Ponde, Goroka Kalakala, Masaki na  Malela. Uongozi wa Tanesco uliahidi kufanya hivyo kwani miradi hii imeshatengewa Bajeti zake. Pia, Tanesco haina uhaba wa vifaa vya kuunganisha umeme kwa sasa.

4. MIRADI MIPYA YA UMEME JIMBO LA KIGAMBONI 

Uongozi wa Tanesco ulinitaarifu kuwa maombi yangu ya kutaka Kata za Kimbiji na Pemba Mnazi kuingizwa kwenye mradi wa Umeme Vijijini (REA) yamekubaliwa na sasa kata hizi zitaanza kupata huduma ya umeme.

Kama nilivyoeleza hapo juu, umeme wa sasa kwa Jimbo la Kigamboni hutoka Ilala, ujenzi wa Sub-Station ya Mbagala unaendelea na unatarajia kukamilika mwezi Disemba, 2014. Kukamilika kwa kituo kutafanya baadhi ya maeneo ya Jimbo la Kigamboni kujitegemea kwa huduma ya umeme na pia kuondokana kukatika katika mara kwa mara kwa umeme kama ilivyo sasa.

Vile vile Tanesco ipo kwenye mchakato wa kutafuta eneo katika Tarafa ya Kigamboni kwa ajili ya ujenzi wa sub-station mpya. Katika mwaka huu wa fedha hakuna fedha iliyotengwa kwa mradi huu. Lengo ni kuingiza ujenzi wa sub-station kwenye bajeti ijayo.

Aidha, niliwataka uongozi wa Tanesco kufanya maandalizi ya awali kujua gharama za kufikisha umeme katika maeneo ya Mwasonga, kata ya Kisarawe II ili makisio haya yaingizwe bajeti ya mwakani. Tulikubaliana zoezi hili kufanyika ndani ya miezi mitatu.

5. HITIMISHO 

Shirika la Tanesco halina uhaba wa vifaa kwa sasa. Niliwataka Tanesco Kigamboni kuandaa mpango kazi wa usambazaji wa huduma ya umeme kwa wateja wapya  ambayo itanisaidia kufuatilia utendaji kazi wao; kuboresha mawasiliano na mahusiano na wateja pindi umeme unapokatika au pale wateja wanapofika kuuliza kuhusu hatma ya maombi yao. Kwa vile, Tanesco ina uhaba wa vikosi vya kuunganisha umeme kwa wananchi, niliwashauri waangalie uwezekano wa kutumia wakandarasi binafsi (outsourcing) baadhi ya kazi hizi.

Kwa wananchi wa Kibada, Toangoma na Gezaulole kwa maeneo mliyoniletea orodha zenu, ndani ya siku 21 nitawapatia majibu ya lini maeneo yanatarajiwa kufikiwa. Aidha, nashauri maeneo husika kuunda kamati ambazo zinashirikiana nami katika ufuatiliaji.

Nawasilisha

Dkt Faustine Ndugulile (MB)

Mbunge Kigamboni

Posted in Uncategorized | Tagged , , , | Leave a comment

Bunge la Katiba-Mjadala wa Rasimu-Siku ya tatu


Leo mjadala wa rasimu umeendelea. Kwa mujibu wa kanuni, kamati zilitakiwa kujadili sura mbili kwa siku mbili. Pamoja na kuongeza siku, baadhi ya kamati zimemaliza kazi na nyingine zimeshindwa kukamilisha kazi hii ndani ya muda uliopangwa.

Tulitarajia kuwa kesho uwasilishaji wa taarifa za kamati ungefanyika Bungeni, lakini kuna dalili zote kuwa Bunge kesho litahairishwa ili kupisha kamati kumaliza kazi zao.

Sura ya kwanza na ya sita zimebeba muundo wa Serikali. Sura hizi ndizo zenye mvutano mkali. Tukifanikiwa kukubaliana kwenye sura hizi, tunatarajia sura nyingine zinaweza kwenda kwa kasi zaidi.

Uwezekano wa kumaliza kazi ya kujadili rasimu ya katiba hii ni mdogo. Kuna uwezekano mkubwa kwa Bunge la Katiba kuahirishwa ili kupisha Bunge la Bajeti kukaa na kupitia Bajeti ya Serikali. Vile vile kuna uwezekano tukashindwa kuendelea iwapo pande zote za Muungano zitashindwa kupata 2/3 ya kura zinazohitajika kupitisha ibara mbali za Katiba.
Wiki mbili au tatu zijazo zitatoa picha halisi ya mchakato huu.

Tuendelee kuwa pamoja.

Posted in Uncategorized | Tagged , , , , | 2 Comments

Bunge la Katiba- Mjadala wa Rasimu-Siku ya Pili


Leo mjadala wa rasimu ya katiba umeendelea, huku mvutano ukiwa katika muundo wa Muungano na vile vile kwa baadhi ya wajumbe kutaka kupatiwa nakala za hati ya Muungano na ushahidi wa kuridhiwa kwa Muungano upande wa Zanzibar. Hata hivyo, vielelezo hivi havikutolewa.

Mzee Pius Msekwa ambaye alikuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati Muungano naye alipata fursa ya kutembelea baadhi ya kamati na kutoa ushuhuda wa matukio mbali mbali kabla na baada ya Muungano.

Tulitarajia kumaliza kupitia sura ya kwanza na sita kesho, lakini kutokana na kazi kuwa kubwa, kesho tutaendelea na kazi hiyo. Kamati nyingi zipo katika ngazi ya kupiga kura, huku mwelekeo unaonyesha Muungano wa Serikali mbili kupewa nafasi zaidi na kuungwa mkono na wengi.

Kesho tunatarajia kukamilisha kazi ya kujadili sura ya kwanza na sita.

Posted in Uncategorized | Tagged , , , , | Leave a comment