Mchango wangu kwenye hotuba ya Waziri Mkuu

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata fursa hii ya kuchangia. Nianze kwa kutoa pongezi kwa watu watatu yaani Katibu Mkuu Ndugu Peniel Lyimo, Mama Nanai na Mzee John Cheyo wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa kazi kubwa na nzuri kwa kushirikiana pamoja na mimi kuhakikisha kwamba fidia ya wahanga wa mabomu katika eneo la Mbagala inalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme, lakini nimeshaanza kupata malalamiko ya wananchi kwamba utaratibu ambao unatumika kuwalipa fedha wahanga hawa si mzuri, wananchi wameshaanza kuhangaishwa. Tumefanya kazi kubwa ya kuzitafuta hizi fedha na kuzifikisha kule kwa wahanga lakini Uongozi wa Mkoa na Uongozi wa Wilaya hawajajipanga vizuri wanawaletea bughudha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nataka nichangie kwa ujumla suala zima la elimu na afya. Mfumo tuliokuwa nao pamoja na ugatuaji wa madaraka katika sekta ya elimu na afya si mzuri inabidi tuuangalie upya. Sekta hizi mbili zinapaswa kuwa ni vipaumbele vya kudumu. Migomo ambayo tunaiona katika hizi sekta kwa kiasi fulani zinachangia na mfumo tuliokuwa nao. Inapaswa tukae tuangalie upya na sisi kama Kamati ambayo inasimamia sekta ya afya na elimu tupo tayari kuwashauri njia bora zaidi ya kuliangalia suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaunga mkono bajeti hii na nitatoa sababu kwa nini siungi mkono bajeti hii.
Mnamo tarehe 16/8/2011 katika bajeti hii na naomba kunukuu kauli ya Mheshimiwa Waziri Mkuu akisema na nanukuu:
“Mheshimiwa Naibu Spika, yapo masuala mazito mazito mengine nimeyasikia atayazungumza…” akimaanisha Mama Tibaijuka. “Lakini naomba mimi kama Waziri Mkuu niyasemee kidogo na hasa hili la Kigamboni na maeneo mengine ya Dar es Salaam ina pilika nyingi sana, nichukue tu dhamana ya kumsaidia Waziri kwa ukubwa wa matatizo ya ardhi yalivyo, sisi tutakachofanya ni kumsihi tu pengine baadaye tukipata nafasi Wabunge wale wote wa Dar es Salaam si vibaya tukakaa pamoja. Hebu tulizungumze jambo hili tuone matatizo yalivyokaa, tuone tunaweza
tukafanya nini kupunguza matatizo yanayozunguka masuala ya ardhi katika Mji wa Dar es Salaam, Dar es Salaam ni eneo dogo ndiyo maana mnaona tunagombana kweli kweli. Tusipojipanga vizuri haitatuletea amani hata kidogo. Kwa hiyo, niko radhi na nitamwomba Waziri naye alipe uzito, nadhani tukikaa na Wabunge hawa tunaweza kabisa tukamaliza vizuri.” Mwisho wa kunukuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kauli ya Waziri Mkuu na alituahidi ndani ya wiki mbili baada ya Bunge la Bajeti kumalizika atakaa na Wabunge wa Dar es Salaam lakini mpaka tunavyoongea hivi sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu hajakutana na Wabunge wa Dar es Salaam. Si kwamba hatumkumbusha, tulimtuma Mwenyekiti wetu zaidi ya mara tatu tukimwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kukutana na Wabunge wa Dar es Salaam. Tumeomba kupitia
wasaidizi wake tukutane na Waziri Mkuu lakini hatujafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam tuna matatizo mengi, kuna suala la UDA. Shirika hili limetolewa bure, sasa hivi mali zake zinauzwa na kutapanywa, viwanja vinauzwa, nyumba zinauzwa,kuna madepo yanauzwa na tunaambiwa kwamba kulikuwa na Tume ambayo iliundwa na Waziri Mkuu kuliangalia suala hili, report hii hatujaipata, wananchi wa Dar es Salaam wanauliza report hii ipo wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala la Jiji la Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam lilivunjwa lakini juzi hapa tena likarejeshwa lakini nasikia tena kuna mchakato wa kulivunja tena. Je, mmekaa na Wabunge wa Dar es Salaam ambao wanawawakilisha wananchi wa Dar es Salaam kuwauliza wanataka nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la mji mpya wa Kigamboni, kwa kweli niseme tu kwamba Serikali inafanya mzaha na suala hili, lakini suala hili ni kubwa. Wananchi wa Kigamboni wamekuwa wanataabika kwa muda wa miaka minne na mpaka sasa hivi Serikali imeshindwa kutoa majibu ya msingi. Tulitarajia kwamba Waziri Mkuu na Waziri husika atakaa na Wabunge wa Dar es Salaam tuweze kukaa na kujadili lakini kwa sababu inaonekana kwamba Serikali imelipuuzia suala hili basi na sisi tutaamua tutakavyofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya fidia ya barabara za Dar es Salaam na mimi hapa nitagusia barabara ya Kilwa. Serikali hii alipokuwa Waziri Shukuru Kawambwa aliwaahidi wananchi wa maeneo ya Temeke na Kigamboni kwamba watalipwa fidia,wavute subira. Alipoingia Waziri Magufuli akasema kwamba hatawalipa fidia na Mheshimiwa Waziri Mkuu hili suala nilikufikishia, iweje Serikali ile ile moja kuwe na kauli zaidi ya mbili? Masuala hayo yote tulikufikishia na mpaka sasa hivi hatujapata majibu na wananchi hawa wamekuwa wanalifuatilia na sasa hivi wanataka kuipeleka Serikali Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kivuko, Serikali ilipandisha bei ya kivuko cha Feri na hili nalo Mheshimiwa Waziri Mkuu tulikufikishia pamoja na kukuandikia barua tarehe 3 Januari, tarehe 13 Januari na kuonana na wewe ana kwa ana tarehe 19 Januari tukakubabidhi barua na mapendekezo ya wananchi wa Kigamboni. Mpaka sasa hivi Mheshimiwa Waziri Mkuu barua zangu hazijajibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunakuja na miradi ya open Government, sasa kama tunashindwa kujibu hata barua hata kuitana, kukaa na kuongea sasa hii open Government tunayoiongelea ni open Government ya namna gani? Ni bora tutoe hizo fedha tukaenda kuziweka katika masuala ya madawati na kuongeza masuala ya madawa, bado hatujafikia level ya kuwa na Open Government.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala ya msongamano Dar es Salaam, sasa hata katika bajeti hii hatuoni kwamba hivi vitu vinapewa kipaumbele. Mkazi wa Dar es Salaam on average anapoteza masaa mawili kwa kila safari yaani masaa manne kila siku.

Sasa sisi ndiyo watu wa Dar es Salaam ambao kwa kweli na sisi inatugusa, uchumi wa Dar es Salaam unadumaa kutokana na msongamano wa barabara zilizokuwepo. Tulitarajia kwamba Mheshimiwa Waziri ungekutana na sisi na sisi tukatoa mapendekezo yetu ya kusaidia jinsi gani ya kusaidia hiki kitu. Lakini yote hayo hayajaweza kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa Mbunge takriban miaka miwili lakini miaka yote miwili pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mkazi wa Dar es Salaam lakini hatujawahi kumuona hata kumsikia siku moja akifanya ziara katika Mkoa wa Dar es Salaam. Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam tumekuona umekwenda Mabwepande, tumekuona katika masuala ya mafuriko lakini hatujawahi kukuona Mheshimiwa Waziri Mkuu ukifanya ziara katika Mkoa wa Dar es Salaam. Wananchi wa Dar es Salaam wanahoji kwamba wamekukosea nini Mheshimiwa Waziri Mkuu?

Kwa nini Mheshimiwa Waziri Mkuu unawafanya wananchi wa Dar es Salaam waonekana wanyonge ilhali na wewe ni mkazi wa eneo lile? Hebu basi panga muda hata kama hutaki kuonana na Wabunge wa Dar es Salaam basi uende ukawatembelee wananchi ili kuwatoa unyonge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani nimalizie hapo sitataka kumaliza muda lakini kwa kweli pasipo na majibu ya kina katika hizi hoja kwa kweli kwetu itakuwa ni ugumu sana, kwa kweli Wabunge wa Dar es Salaam tumesema kwamba hapana, hii bajeti hatuiungi mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia hapo.

Advertisements

About Dr Faustine Ndugulile

#Medical Doctor #Microbiologist # Public Health Specialist #Politician #African #Proud Tanzanian
This entry was posted in Uncategorized. Bookmark the permalink.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s