Baraza jipya la mawaziri na tatizo la mfumo

Hatimaye lile baraza jipya la mawaziri lililokuwa likisubiriwa kwa hamu, limetangazwa jana. Mabadiliko haya yanakuja baada ya Bunge kutishia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu. Kwa kiasi kikubwa, Mheshimiwa Rais amezingatia maazimio ya kamati ya Chama Cha Mapinduzi katika Bunge, kuwaondoa madarakani mawaziri walioguswa na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali na wale ambao wizara zao zinatuhumiwa kwa ubadhirifu.

Pamoja na kuipongeza timu hii mpya, vile vile nataka kuwapa pole. Timu hii inaingia kwenye baraza la mawaziri (BLM) katika kipindi kigumu sana. Inabidi timu hii ifanye kazi kubwa ya kurejesha imani na matumaini kwa wananchi. Timu hii inakabiliwa na changamoto zifuatazo.

Kwanza, wizara nyingi zinakabiliwa na ukata mkubwa sana wa fedha, wizara na taasisi nyingi zinajiendesha kwa kusuasua na miradi mingi ya maendeleo imekwama. Bila kwa wizara kuwezeshwa, mawaziri watalaumiwa bure.

Pili, tuna tatizo la kimfumo ndani ya Serikali na hili ndio tatizo kubwa. Mawaziri wengi walioachwa kwenye BLM, imebidi kuwajibika kisiasa kutokana na watendaji walio chini yao kuharibu kazi. Tusiporekebisha tatizo la mfumo uliopo wa Serikali, kila mwaka tutakuwa tunawafukuza mawaziri.

Matatizo ya kimfumo ni yapi?

Mosi, mamlaka ya uteuzi wa mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi wa wizara, wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu ni Rais. Katika miaka ya karibuni, tumeshuhudia ngazi hizi za utawala kutoheshimiana na kufanya kama kazi timu moja. Mfumo wa uteuzi wa kada hizi unabidi uangaliwe upya na kubadilishwa.

Pili, kwa mfumo wa sasa, waziri ni kiongozi wa kisiasa na kisera ndani ya wizara. Mamlaka ya watumishi na fedha yako kwa makatibu wakuu ambao ndio watendaji wakuu. Katibu Mkuu asipompenda waziri anaweza kufanya maisha yake ndani ya wizara kuwa magumu. Mawaziri wengi wamekuwa ombaomba ndani ya wizara zao. Hivi karibuni, tumeona makatibu wakuu wakitengeneza mtandao ndani na nje ya Serikali. Ukitaka kuthibitisha kauli, angalia bodi za taasisi kubwa na zenye maslahi, utaona wenyeviti wake wengi ni makatibu wakuu wastaafu.
Inapaswa mahusiano kati ya mawaziri na makatibu wakuu, wakurugenzi, bodi na watendaji wa taasisi uangaliwe upya kwa nia ya kuleta ufanisi na uwajibikaji. Mawaziri wapewe mamlaka ya wakuwajibisha watendaji chini yao.

Mwisho, Mfumo uliopo kwa Serikalini ni mpana, wenye urasimu mwingi na usioendana na mahitaji na matakwa ya zama hii ya sayansi na teknolojia. Mfumo huu unahitaji kufanyiwa maboresho makubwa ili uwe rafiki, kuleta ufanisi na tija kwa maendeleo ya nchi yetu.

Narudia tena, tusipoangalia matatizo ya kimfumo na kuyarekebisha, mawaziri wataendelea kutuhumiwa na kulaumiwa. Turekebishe hili, ili tuweze kuwawajibisha vizuri.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania

About Dr Faustine Ndugulile

#Medical Doctor #Microbiologist # Public Health Specialist #Politician #African #Proud Tanzanian
This entry was posted in Uncategorized. Bookmark the permalink.

Leave a comment