Sakata la Kivuko-Barua ya Pili kwa Waziri Mkuu

BUNGE LA TANZANIA

OFISI YA MBUNGE WA JIMBO LA KIGAMBONI

Kumb na: KIG/KVK/VOL.1/7 13 Januari 2012

Mhe. Mizengo Peter Pinda (MB)
Waziri Mkuu
DAR ES SALAAM

YAH: ONGEZEKO LA VIWANGO VYA NAULI KATIKA KIVUKO CHA MAGOGONI
Kichwa cha habari hapo juu chahusika.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, mnamo tarehe 03 Januari 2012 nilikuandikia barua yenye kumbukumbu KIG/KVK/VOL.1/6 nikiomba uingilie kati katika suala la ongezeko la nauli katika kivuko cha Magogoni zilizoanza kutumika tarehe 01.01.2012. Barua hii haijajibiwa, hivyo kunilazimu kuandika barua hii ya kukumbushia.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, hoja ya wanaKigamboni haikuwa kwenye ukubwa au udogo wa Tsh 200 kama inavyopotoshwa kwenye vyombo vya habari. Hoja za wanakigamboni zipo kwenye mambo yafuatayo:
a. Wananchi wanataka kuelewa mchakato na vigezo vilivyotumika kufikia nauli mpya.
b. Katika dhana ya utawala bora na ushirikishwaji umma kwenye mambo yanayowahusu wananchi, kwanini wakazi wa Kigamboni hawakushirikishwa kwenye mchakato huu pamoja na kuomba kushirikishwa. Rejea barua yangu ya tarehe 19 Januari 2011 kwenda TEMESA kuhusiana na suala hili.
c. Kukosekana uwazi na taarifa za mapato na matumizi katika kivuko hiki.
d. Kivuko ni huduma na sio biashara. Ongezeko kubwa la nauli linaonekana kulenga kuwakomoa watumiaji wa kivuko hiki.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na hoja nilizoainisha kwenye barua yangu ya awali kwako, ni dhahiri kuwa viwango vipya vya nauli havikufanyiwa utafiti wa kutosha na madhara yake yameshaanza kujitokeza tangu nauli mpya zianze kutumika:
1. Wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 ambao awali walikuwa na msamaha sasa hivi wanalipishwa Tsh 200.
2. Watoto chini ya miaka 14 hata kama ni mchanga aliyezaliwa leo wanalipishwa Tsh 50.
3. Vyakula vingi vinasafirishwa kwa baiskeli za miguu mitatu (maguta) na mikokoteni toka mjini kuja Kigamboni. Ongezeko la nauli kwa vyombo hivi vya usafiri vimeongezeka maradufu gharama za vyakula katika maeneo ya Kigamboni na anayeathirika ni mlaji. Nauli za awali na mpya ni kama zifuatazo:
a. Guta toka Tsh 200 hadi Tsh 1800 (Asilimia 800); bei ambayo ni kubwa kuliko ya gari ndogo.
b. Bajaj zimepanda toka Tsh 300 hadi Tsh 1300 (asilimia 333).
c. Mikokoteni imeongezeka toka Tsh 200 hadi Tsh 1500 (Asilimia 650).
4. Pamoja na kupanda kwa asilimia kubwa kwa nauli ya maguta, pikipiki na Bajaj, bado mizigo inayobebwa na vyombo hutozwa nauli. Mzigo chini ya Kg 50 hulipishwa Tsh 200 na zaidi ya 50 Kg hulipa Tsh 500. Ulipishaji wa mizigo umeleta usumbufu mkubwa sana na kupandisha gharama za maisha. Aidha, wanakigamboni wanaokwenda kununua kitoweo kwenye soko la samaki Magogoni wanaporudi Kigamboni, kitoweo hiko nacho hutozwa nauli. Vile vile kina mama na vijana wanaojishughulisha na biashara ndogo navyo hutozwa nauli kulingana na ujazo wanapovuka kufanya biashara. Malipo haya ya mizigo pia yanalalamikiwa na wanakigamboni kwa sababu mamlaka ya kivuko haina mizani, hivyo ukubwa wa mzigo ni kwa njia ya kukadiria.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, bado naendelea kusisitiza ukusanyaji na uthibiti wa mapato kwenye kivuko hiki bado ni changamoto hata baada ya kubadilisha uongozi, kufukuza baadhi ya watumishi na kuimarisha ulinzi. Wanakigamboni wanaamini ikiwa mapato na matumizi yatadhibitiwa vizuri, fedha ya kutosha ingepatikana kuendesha vivuko na hata kama kuna pengo, viwango vya nauli visingepanda kufikia vya sasa.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, wanakigamboni wameonyesha uvumilivu wa hali ya juu sana. Pamoja na maneno ya kejeli na ubabe yaliyotolewa na viongozi waandamizi wa Serikali, wananchi hawa wameendelea kuwa wavumilivu wakiamini suala hili linashughulikiwa. Ukimya wao sio kwamba wameridhika na viwango vipya vya nauli.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninashauri uziite pande zote zinazohusika katika suala hili kufikia muafaka. Kama mwakilishi wa wananchi wa Kigamboni nipo tayari wakati wowote ule nitakapohitajika.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, pamoja na mapendekezo yangu kwenye barua yangu ya awali kwako, nawasilisha rasimu ya mapendekezo yetu kuhusiana na viwango vya nauli.

Mwisho, Mheshimiwa Waziri Mkuu, wanakigamboni wanaamini Serikali yao ni sikivu, itasikia kilio chao na kuchukua hatua za haraka.
Wako katika ujenzi wa Taifa

Mhe. Dkt Faustine Ndugulile (MB)
MBUNGE
Nakala:
1. Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
2. Mhe. John Magufuli-Waziri wa Ujenzi
3. Mhe. Mecky Sadick-Mkuu wa Mkoa Dar Es Salaam
4. Kamati ya Wabunge wa Dar Es Salaam
5. Waheshimiwa Madiwani wote-Jimbo la Kigamboni

Advertisements

About Dr Faustine Ndugulile

#Medical Doctor #Microbiologist # Public Health Specialist #Politician #African #Proud Tanzanian
This entry was posted in Uncategorized. Bookmark the permalink.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s