Barua kwa Waziri wa Ujenzi kupinga ongezeko la nauli ya kivuko (Kivukoni-Kigamboni)

BUNGE LA TANZANIA

OFISI YA MBUNGE WA JIMBO LA KIGAMBONI

 

Kumb na: KIG/KVK/VOL.1/4                                                                  29 Disemba 2011

Mhe. Dkt John P. Magufuli (MB)

Waziri

Wizara ya Ujenzi

Dar es Salaam

YAH: KUSUDIO LA ONGEZEKO LA VIWANGO VYA NAULI KATIKA KIVUKO CHA KIVUKONI-KIGAMBONI

Kichwa cha habari hapo juu chahusika.

Wananchi wa Jimbo la Kigamboni wamepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kusudio la kuongeza nauli za abiria, magari na vyombo vingine vinavyotumia huduma ya kivuko kati ya Kigamboni na Kivukoni kuanzia tarehe 1 Januari 2012.

Kivuko hiki ni kiungo muhimu kwa wananchi wanaoishi upande wa Kigamboni ambao wengi wao ni watu wa kipato duni na hawana ajira za kudumu.  Ongezeko la nauli kwa asilimia 100 ni kubwa sana na litawaathiri kiuchumi. Nimepigiwa simu nyingi na kuletewa malalamiko mengi katika siku ya leo kuhusiana na mpango huu wa kuongeza nauli. Wananchi wanataka kujua ni vigezo gani vilivyotumika kufikia nauli hizi mpya; vyombo gani vilivyopendekeza, kupitisha na kuidhinisha nauli hizi na wanataka kujua kwa nini hawakushirikishwa katika mjadala wa nauli mpya.

Pamoja na ongezeko kubwa la wakazi na magari yanayotumia huduma ya kivuko, cha kushangaza ni kwamba mapato kwa siku yamekuwa ni takribani Tsh 8 milioni kwa siku kwa muda mrefu sasa.

Ni dhahiri kumekuwa na upotevu mkubwa mikononi kwa watumishi wasio waaminifu wa kivuko.  Mapato mengi yanapotea kwa njia zifuatazo:

 1. Baadhi ya watumishi wa kivuko kukatisha risiti hususan za magari kwa kutumia vitabu bandia.
 2. Baadhi ya watumishi kuziuza tena tiketi zilizotumika badala ya kuzichana.
 3. Baadhi ya watumishi na askari wanapitisha magari na abiria baada ya kupokea malipo ya pembeni.

Vilevile mafuta ya vivuko huuzwa kwa wavuvi wadogo wadogo katika maeneo ya Feri.

Mambo haya yote yanafanyika pasipo kificho, binafsi nimeshawahi kushuhudia yote niliyosema hapo juu yakifanyika na kuyatolea ripoti kwa uongozi wa kivuko.

Ninaamini kuwa hatua zifuatazo zikichukuliwa mapato ya kivuko hiki yanaweza kufika zaidi ya Tsh 13 milioni kwa siku:

 1. Kudhibiti uuzaji wa tiketi  za abiria na magari.
 2. Kudhibiti ununuzi, utunzaji na matumizi ya mafuta yanayotumika kwenye vivuko.
 3. Kudhibiti idadi ya watu na magari yanayovuka bila kulipia huduma hii.
 4. Kupunguza gharama za uendeshaji ikiwa ni pamoja na kupunguza idadi ya vibarua.

Kutokana na unyeti wa suala hili, nashauri zoezi hili lisitishwe ili kutoa fursa ya kujadiliana kuhusu upandishaji wa nauli na maboresho ya huduma hii kwa kushirikiana na wadau na wawakilishi wa wananchi katika Jimbo la Kigamboni.

Natumaini mapendekezo haya yatafanyiwa kazi ili kuepuka kuwabebesha mzigo wa gharama za uendeshaji wakazi wa Kigamboni wanaotumia huduma ya kivuko pale Feri.

Naambatanisha nakala ya barua yangu ya tarehe 19 Januari 2011 yenye kumbukumbu namba KIG/KVK/VOL.1/1 kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TEMESA ambayo ilitoa mapendekezo ya njia ya kuboresha huduma na vile vile kutaka ushirikishwaji wa wadau katika suala la ongezeko la nauli. Barua hii haijajibiwa hadi hivi sasa.

Natanguliza shukrani zangu za dhati.

Wako katika ujenzi wa Taifa

Mhe. Dkt Faustine Ndugulile (MB)

MBUNGE

Nakala:

 1. Mhe. Mizengo Pinda (MB)-Waziri Mkuu
 2. Mhe. Mecky Sadick-Mkuu wa Mkoa Dar Es Salaam
 3. Waheshimiwa Madiwani wote-Jimbo la Kigamboni
 4. Wenyeviti wa Serikali za Mitaa-Jimbo la Kigamboni
 5. Mkurugenzi Mkuu-TEMESA

About Dr Faustine Ndugulile

#Medical Doctor #Microbiologist # Public Health Specialist #Politician #African #Proud Tanzanian
This entry was posted in Uncategorized. Bookmark the permalink.

One Response to Barua kwa Waziri wa Ujenzi kupinga ongezeko la nauli ya kivuko (Kivukoni-Kigamboni)

 1. Rashid says:

  Sio sawa serikali kubadilisha nauli za kivuko bila kutoa ufafanuzi wowote kuhusu sababu za mabadiliko kwa wananchi. Huo ni udiktekta. Mapato yanayokusanywa sasa hayana ufafanuzi yanatumikaje. Huduma imeshazidiwa na ongezeko la watu kwavile sehemu za kusubiria pantoni huzidiwa na watu na hakuna hata hewa ya kutosha kwavile pembeni ya jumba, mfano upande wa magogoni kumejengwa vibanda vya ulevi na vinakinga hewa. Paa la jengo hilo lingetakiwa kuwa na ‘ridge ventilator’ ili hewa iwe nzuri. Kukata tiketi ni foleni (msongamano) mkubwa na wakati mwingine unanyeshewa na mvua. Abiria wanajazana hadi sehemu yanapokaa magari ndani ya pantoni kitu ambacho si salama. Suluhisho la matatizo ya kivuko ni kujenga daraja. Kwanini suala la daraja linakuwa hadithi? Mapato yote ya kilasiku katika kivuko yanatumikaje?

  Like

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s