Mchango wangu katika taarifa ya hali ya uchumi wa Taifa 2011/2012

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia bajeti hii. Awali ya yote, napenda kuwashukuru Wana-Kigamboni kwa kunichagua kuwa Mbunge wao, nawaahidi uwakilishi uliotukuka na kamwe sitowaangusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kusikia kilio cha wananchi. Kabla ya kuja katika Bunge hili, nilipita katika baadhi ya Kata zangu katika Jimbo la Kigamboni na kilio kikubwa ni kwamba bajeti hii isikilize kilio cha wananchi cha hali ngumu ya maisha. Niipongeze Serikali kwa kuliona hilo na kutengeneza bajeti ambayo imeliangalia hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, niipongeze Serikali kwa kutengeneza bajeti ambayo imezingatia vipaumbele vya Kitaifa. Mheshimiwa Mnyika wakati anatoa hoja yake alisema kwamba zile ahadi ambazo walikuwa wameahidi katika Ilani yao kwamba ni lazima zitengenezwe pre-conditions ya kuzifanikisha. Vilevile kwa huu Mpango ambao Serikali umekuja nao na sisi tunatengeneza hizo pre-conditions za ku-take off ili ile dhana nzima ya maisha bora kwa kila Mtanzania iweze kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nijikite katika baadhi ya maeneo. Vipaumbele ambavyo vimeainishwa katika bajeti yetu ni vya msingi lakini vilevile nataka kuongeza kwamba kuna hatua kubwa ambayo tumepiga katika suala la afya na elimu. Mafanikio haya yanapaswa kulindwa na napendekeza kwamba pamoja na hivi vipaumbele ambavyo tumeviweka hapa suala la elimu na afya viwe ni vipaumbele vya kudumu. Mtaji wa maskini ni elimu na afya njema aliyokuwa nayo. Niipongeze tena Serikali kwa Mpango wa Maendeleo ambao tuliuidhinisha hivi karibuni. Tunaomba sana Serikali hii iwe ndiyo dira ya uandaaji wa bajeti zetu na kuwepo na mwendelezo. Lile wazo ambalo tumekuwa nalo la kuanzisha Ofisi ya Bajeti katika Bunge litasaidia sana kulipa Bunge letu mwongozo katika uandaaji na ufuatiliaji wa bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia kidogo katika masuala ya ugumu wa maisha. Kuna masuala matatu ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia sana katika kuleta hali hii tuliyonayo ya ugumu wa maisha. Moja, ni suala la mafuta, pili, suala la umeme na tatu ni suala la bei za vyakula. Serikali imeonesha nia njema kabisa ya kutaka
kupunguza kodi na tozo katika suala la mafuta, hii ni hatua nzuri. Ni hatua ambayo ningemwomba ndugu yangu Mhe. John Mnyika asiibeze, ndio pre-conditions ambazo tunaziongelea. Serikali imesema kwamba itaiangalia suala hili ili kati ya zile tozo na kodi mbalimbali ni zipi ambazo inaweza kupunguza kuleta unafuu katika bei ya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumeongelea kwamba kuna utaratibu ambao tunataka tuuanzishe wa bulk procurement ya mafuta, mfumo huu utapunguza sana gharama za mafuta. Vilevile kuna mambo ambayo tunahitaji tuyaangalie pamoja na hatua nzuri ambazo tumezichukua, bado udhibiti wa bei za mafuta nchini sio mzuri.
Tunaandika katika magazeti kwamba bei ya mafuta katika kila Mkoa isizidi kiasi fulani lakini bado tunaona kwamba upandishwaji wa bei ya mafuta ni holela. Serikali bado inahitaji kulifanyia kazi suala hili. Pili bado tunahitaji kudhibiti ubora wa bidhaa za mafuta, uchakachuaji wa mafuta uko juu sana. Hii inatutia hasara kubwa sana na ni suala kwa kweli bado tunahitaji tuliangalie vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme ni janga la Kitaifa nadhani wasemaji wengi waliopita wameliongelea. Hatuhitaji siasa katika suala la umeme. Wananchi waliotutuma wanahitaji kuona vitendo zaidi. Tuwe na malengo thabiti na tuweke muda maalum wa utekelezaji. Vilevile twende mbele zaidi pale malengo yasipotimia tuwe na njia ya uwajibikaji ili tufike mahali kwamba hili tatizo la umeme liwe ni historia. Bajeti iliyotengwa katika sekta hii bado ni ndogo sana kuondoa kabisa tatizo hili. Kwa hiyo, ni suala la umeme tunahitaji tukae tulitafakari kwa kina kwa kuangalia jinsi gani tunaweza tukaboresha ili basi ndani ya hii miaka mitano tatizo la umeme liweze kuondoka kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la chakula, tunaishukuru Serikali na kuipongeza kwamba iliweza kutoa mahindi katika Ghala la Taifa au Hifadhi ya Taifa kwa ajili ya kupunguza tatizo la njaa lililokuwepo na ikatoa bei ambayo ilipaswa kutumika katika kuuza ule unga, lakini bado tuna haja ya kuwa na utaratibu wa kudhibiti bei za vyakula muhimu kwa wananchi. Ikiwezekana turudishe Tume ya Bei ili bei ya vitu kama unga, mchele, maharage na sukari viweze kuthibitiwa. Nakumbuka hapa katikati bei ya sukari ilipanda sana, Waziri Mkuu akatoa tamko kwamba sukari isiuzwe zaidi ya shilingi 1,700/=, lakini ukivuka kwenda Kigamboni bei ya sukari pale ni shilingi 2,000/=. Kwa hiyo, kwa kweli bado tunahitaji jitihada za makusudi kufanyika ili kuhakikisha kwamba bei za vyakula zinadhibitiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee katika vyanzo vya mapato na matumizi. Kama tuna nia ya dhati ya kuleta maendeleo nchini basi bajeti zetu zinatakiwa kuonesha mlengo huo. Suala la kudhibiti matumizi yasiyo lazima, matumizi mabaya na upotevu wa fedha yanahitaji kufanyiwa kazi. Tunashukuru Serikali imeanza kuonesha nia hiyo ya kudhibiti baadhi ya matumizi lakini suala la Hati Chafu ambazo zinapatikana katika baadhi ya Taasisi na Halmashauri, zinanipa mashaka makubwa sana. Kuna upotevu mkubwa sana wa fedha, hili linahitaji kudhibitiwa. Wakati tunataka kuonesha kwamba tuna nia ya dhati ya maendeleo basi na sisi tuonekane tunajibana. Kuna matumizi mengine ambayo sio ya lazima ambayo inabidi kuyaangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka kulisemea kidogo ni suala la matumizi ya Dola katika uchumi wetu. Tanzania sasa hivi inakuwa kama Zimbabwe. Tuna shilingi yetu lakini vitu vingi sasa hivi tunatumia Dola katika manunuzi. Suala hili linahitaji kudhibitiwa. Mimi si Mchumi lakini nadhani suala hili lina athari kubwa sana katika thamani ya fedha zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwamba sasa hivi tuna mfumuko mkubwa sana wa maduka ya fedha za kigeni, haya nayo yanahitaji kudhibitiwa. Maduka haya yanatumika kuhalalisha fedha haramu na utoroshaji wa fedha zetu nje ya nchi. Tunahitaji kusimamia vizuri maduka haya ambayo yanabadilisha fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuendelea, lazima tupanue wigo wa kodi. Wigo wetu wa kodi bado ni mdogo sana. Nilikuwa naangalia uwiano wa kodi na pato la Taifa, kodi inachangia karibu asilimia 16.3, hii bado ni ndogo sana, wenzetu Kenya sasa hivi wako zaidi ya asilimia 20, tunahitaji kushirikisha sekta zisizo rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hatujaweza kukaa na kutumia kikamilifu jiografia ya nchi yetu na rasilimali tulizokuwa nazo. Sasa hivi ukiangalia pamoja na bandari tuliyokuwa nayo, nchi ambazo ziko jirani na sisi wanaanza kutukimbia. Wanatumia bandari ya Mombasa na juzi nilikuwa nasoma kwamba wenzetu wa Zambia wameanza kuwekeza katika bandari ya nchi kavu kule Namibia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya uvuvi nayo kwa kweli ni eneo ambalo tunahitaji kukaa na kulifanyia kazi kwa haraka. Mchango wake katika pato la Taifa ni asilimia 1.4, bado ni dogo sana. Tunahitaji kuwekeza katika sekta hii na ikiwezekana si dhambi kuifufua tena TAFICO ili basi itusaidie katika eneo hili la kuongeza pato la Taifa na vilevile kuongeza katika ajira kwa vijana. Mifugo tunayo mingi sana, tuna ng’ombe karibu 20,000,000 na mbuzi 13,000,000 tukiweza kuitumia vizuri rasilimali hii kwa mauzo ya nyama, jibini, maziwa na ngozi kama wenzetu wa Botswana, tunaweza tukapata pato kubwa la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile matumizi ya ardhi bado ni madogo sana. Eneo la ardhi inayolimika ni karibu asilimia 23 ya nchi hii lakini ukikaa ukiangalia kilimo cha umwagiliaji tunatumia asilimia moja tu. Katika hotuba nyingi za wenzangu wamekuwa wakichangia kuhusu masuala ya njaa. Tuna vyanzo vingi vya maji ambavyo tukiweza kuvitumia vizuri vinaweza vikatusaidia kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo kuhusu suala la Kigamboni. Naishukuru Serikali kwa kuweza kusikia vilio vyetu Wana-Kigamboni, ahadi za Rais ndani ya miezi sita zimeanza kutekelezwa. Ujenzi wa daraja la Kigamboni utaanza mapema mwakani na ujenzi wa barabara ya Kilwa umeanza, tumeanza vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala la Mji Mpya wa Kigamboni. Tunaiomba Serikali ichukue hatua za haraka za kuanza ujenzi wa Mji wa Kigamboni. Wana-Kigamboni wako tayari lakini kadri Serikali inavyochukua muda inazidi kuwatia umaskini. Wana-Kigamboni hawakopesheki, hawawezi kuendeleza wala kuuza ardhi yao na nyumba zao, Wana-Kigamboni wanahitaji kutoka kifungoni kwa Serikali kuwaambia ni lini mradi huu utaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihitimishe kwa kusema kwamba nchi yetu inasifika kwa amani na utulivu. Kuna wenzetu wanalilia na kutamani amani na utulivu tuliokuwa nao, sisi tunaanza kuichezea. Wananchi waliotutuma ni waajiri wetu wanaotaka kuona humu ndani ya Bunge tunakuwa na mijadala ya kuleta maendeleo na ustawi wa nchi yetu na kuboresha maisha yao. Mambo ya mipasho, malumbano na vijembe hayafai. Siasa sio uadui na wala siasa sio uhasama. Tofauti za itikadi ni
mtazamo tofauti wa kufikia lengo lilelile moja na kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi).

Dr Faustine Ndugulile

Mbunge-Kigamboni

16 Juni 2011

About Dr Faustine Ndugulile

#Medical Doctor #Microbiologist # Public Health Specialist #Politician #African #Proud Tanzanian
This entry was posted in Uncategorized. Bookmark the permalink.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s