Mchango wangu kwenye hotuba ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuchagia katika Hotuba hii ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira). Mengi yamesemwa kuhusiana na suala hili la Muungano, lakini ninadhani ni jambo jema kadiri muda unavyokwenda na sisi tuweze kufanya tafakari.

 Mheshimiwa Naibu Spika, wazee wetu wa zama za enzi za mawe, walikuwa wanatumia zana za mawe lakini na wao waliweza kufanya tafakari ya jinsi gani wanaweza wakaboresha maisha yao ili maisha yao yaweze kwenda vizuri. Vilevile wazee wetu ambao walipigania uhuru wa nchi hii wangeweza kuridhika kula, kulala na kuvaa katika mazingira ya ukoloni, lakini nao waliweza kutafakari na kuona kwamba, maisha yao yanaweza yakawa bora zaidi.

 Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kusema kwamba, kuhoji siyo dhambi na kufanya tafakari siyo dhambi, kwa sababu tangu Muungano wetu mwaka 1964, tunafikia karibu miaka hamsini sasa. Ili kuboresha zaidi Muungano wetu, tunahitaji tukae na tuuangalie upya jinsi gani tunaweza tukaondoa hizi kero. Kero ni nyingi kama zilivyoainishwa na baadhi ya wasemaji waliopita.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Katiba ya Zanzibar, ambayo imeandikwa mwaka 2010, imeainisha baadhi ya maeneo ambayo yanahitajiwa sasa yaoanishwe na Katiba mpya ambayo tutaiandika. Tulipoungana mwaka 1964, tulisema kwamba, tunaungana kutengeneza nchi moja, lakini Katiba Mpya ya Zanzibar, imemtaja Rais wa Zanzibar kama Mkuu wa nchi, imetaja mamlaka ambayo Rais wa Zanzibar atakuwa nayo pamoja na kugawa mikoa. Vilevile imetaja kwamba, Mahakama ya Rufaa haitakuwa na maamuzi katika suala la Zanzibar.

 Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna changamoto nyingine ambazo zipo; mfano ni hizi ambazo tumeziongelea; mgawanyo wa mapato na rasilimali, mfumo wa kodi, umiliki wa mali na uwakilishi katika vyombo mbalimbali vya dola. Sasa tunakaribia miaka hamsini, lengo letu ni kuboresha na kuuimarisha huu Muungano wetu. Kwa hiyo, ninatoa ushauri kwamba, wakati tunaendelea na huu mchakato wa kujadili Katiba Mpya, ninadhani ni wakati mwafaka tukatumia fursa hii kujaribu kukaa na kuangalia huu muundo wa Muungano uwe wa namna gani na aina ya Muungano ambao tunataka tuwe nao. Hii itatusaidia sana sisi ili tutakapokuwa tumefanya maamuzi kwa kuwashirikisha na Wananchi wetu, basi muundo na aina ya Muungano utakaokuwepo, uweze kuwa na tija kwa pande zote mbili, tuangalie kwamba kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama muundo wetu wa Muungano uwe namna gani.

 Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kugusia kidogo katika masuala ya Mazingira. Waziri husika ameelezea vizuri sana katika hotuba yake ya nini Wizara yake imekuwa inafanya, lakini kuna programu nyingi sana ambazo amezigusia katika kitabu chake cha hotuba. Tatizo langu ambalo ninaliona siyo wingi wa programu ambazo zipo zimeainishwa au ubora wa zile nyaraka, tatizo letu lipo zaidi katika utekelezaji.

Bado tuna tafsiri mbovu au potofu ya nini maana ya utunzaji wa mazingira, watu wengi tunafikiria kwamba, utunzaji wa mazingira ni pale tu inapohusisha upandaji wa miti na hii inajionesha wazi hata katika zile Sherehe za Kitaifa, ambazo tumekuwa tunazifanya mara nyingi tunaishia kupanda miti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mambo ambayo yanaendelea hivi sasa katika nchi yetu ambayo kwa kweli yanatishia mustakabali wa nchi yetu. Miti bado inaendelea kukatwa ovyo, biashara ya mkaa ambayo miaka ya nyuma tulisema kwamba, tutaidhibiti bado inaendelea kwa kasi, tumekuwa tunaongelea masuala ya mabadiliko ya tabianchi na haya yameshaanza kujidhihirisha taratibu. Sasa hivi tunaongelea kwamba kina cha Ziwa Tanganyika kinazidi kupungua, theluji juu ya Mlima Kilimanjaro inapungua, misimu ya mvua sasa hivi nayo imeanza kubadilika na inawezekana kabisa hili baa la njaa ambalo linatunyemelea, pamoja na mgawo wa umeme nao unaweza ukawa unachangiwa na haya mabadiliko ya tabianchi.

 Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumekuwa na uingizaji mkubwa sana wa vifaa chakavu kutoka nje ya nchi. Sasa hivi ukipita hata hapa Dodoma, Dar es Salaam na mikoa mingine mikubwa, kuna majokofu mengi sana ambayo mengi hayapo CFC free, pamoja na kompyuta na zana zingine za electronics. Inafaa sasa tukaanza kuviangalia vifaa hivi na ikiwezekana, sheria kali ziweze kutungwa za kudhibiti uingizaji wa vifaa hivyo.

 Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ninataka kuliongelea ni kwamba, katika Pwani zetu sasa hivi uvuvi haramu unashika kasi kubwa sana. Kule Kigamboni, kuanzia Kigamboni, Mjimwema, Somangila, Kimbiji mpaka Pemba Mnazi, kila siku tunasikia milio ya mabomu, tukiacha hili likaendelea,uvuvi haramu utapunguza sana mazalia ya samaki na kutafanya sasa wavuvi wetu ambao walikuwa wanaweza kupata samaki katika maeneo ya karibu, waende mbali zaidi.

 Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Wizara husika nao waweze kuliangalia suala la uvuvi haramu na ikiwezekana waweze kuboresha vitengo ambavyo vinasimamia suala hili ili viweze kudhibiti hali hiyo.

 Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwamba, baadhi ya viwanda na migodi inachafua mazingira na vyanzo vya maji. Mengi yamesemwa lakini ninaomba nami nigusie jambo langu moja katika eneo langu la Kigamboni. Katika eneo la Vijibweni, kuna eneo linaitwa Kidongoni, kuna kiwanda cha gesi kinaitwa Mihan; kiwanda hiki kimejengwa katika maeneo ya makazi ya watu, kinatoa harufu kali na mara kwa mara hata mimi juzi nimepita pale mitungi ya gesi ilikuwa inalipuka na Wananchi hawa wametoa taarifa katika sehemu zote zinazohusika, wamekuja Wizara ya Mazingira, wamekwenda Manispaa, wamekwenda NEMC, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa. Wananchi hawa wanaishi kwa wasiwasi mkubwa sana.

 Mheshimiwa Naibu Spika, ninamwomba Waziri wa Mazingira, apate fursa aende akajionee hali halisi ambayo Wananchi wa Kidongoni Vijibweni wanakabiliana nayo na hali ya mashaka iliyopo katika kile kiwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbagala pia kuna kiwanda cha KTM na kiwanda cha simenti. Kwa taarifa ambazo zipo, inasemekana kwamba, hata hati ya Environmental Impact Assessment hususan katika hiki kiwanda cha simenti ni ya mashaka. Vilevile mfumo wa maji taka kutoka katika viwanda hivi viwili imeelekezwa katika makazi ya watu. Ninaomba Waziri tutakapokuwa tunafanya ziara, basi tuweze kupita na kuliangalia suala hili.

 Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ninataka kuligusia ni hili la mifuko ya plastiki. Serikali imesema kwamba, mifuko ya plastiki ambayo inapaswa kutumika nchini ni ile ambayo ina unene usiozidi micron 30. Sasa hii lugha ni ya kitaalamu sana kwa sababu hata mimi Mbunge ukiniuliza mfuko wenye unene wa micron 30 siujui na wala siufahamu, nina uhakika kabisa hata Wananchi wa kawaida kule mtaani nao pia hawalielewi vizuri suala hili.

 Mheshimiwa Naibu Spika, ili kudhibiti hali hii kwa nini Serikali isitoe tamko kwamba tunafuta matumizi ya mifuko ya plastiki na badala yake tukaweza mifuko ya karatasi ili tuondokane kabisa na dhana hii kwani mifuko hii kwa kiasi kikubwa sana inachafua sana mazingira katika maeneo yetu. Katika Hotuba ya Waziri amegusia kwamba, katika usimamizi wao wameweza kutembelea Mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, na Mbeya; hii haitoshi, bado elimu inahitajika kwa Wananchi na bado usimamizi unahitajika kuboreshwa na ikiwezekana tuifute kabisa mifuko hii ili tuweze kutumia mifuko ya karatasi.

 Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ninaomba nitoe rai kwa Serikali, majukumu ya Wizara ya Mazingira ni makubwa na ya msingi kwa mustakabali wa nchi yetu, lakini nyenzo zilizopo hazitoshi. Kwa hiyo, kuna haja ya kuboresha na kuongezea bajeti ya Wizara hii na kuwajengea uwezo Halmashauri ili ziweze kusimamia vyema Sheria ya Mazingira na utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya machache, ninashukuru sana. (Makofi)

Dr Faustine Ndugulile-Kigamboni MP

08/07/2011

 

Advertisements

About Dr Faustine Ndugulile

#Medical Doctor #Microbiologist # Public Health Specialist #Politician #African #Proud Tanzanian
This entry was posted in Uncategorized. Bookmark the permalink.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s